1 Timothy 3

Sifa Za Waangalizi

1 aHili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kazi ya uangalizi, atamani kazi nzuri. 2 bBasi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, 3 casiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. 4 dLazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia. 5 e(Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?) 6 fAsiwe mtu aliyeokoka karibuni asije akajivuna na kuangukia kwenye hukumu ile ile ya ibilisi. 7 gInampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi.

Sifa Za Mashemasi

8 hVivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali. 9 iInawapasa kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamiri safi. 10 jNi lazima wapimwe kwanza; kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi na waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi.

11 kVivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasio wasingiziaji, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo.

12 lShemasi awe mume wa mke mmoja na inampasa aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema. 13 mWale ambao wamehudumu vyema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Al-Masihi Isa.

14Ingawa ninatarajia kuja kwako hivi karibuni, ninakuandikia maagizo haya sasa ili kwamba, 15 nkama nikikawia, utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo kanisa la Mungu aliye hai, lililo nguzo na msingi wa kweli. 16 oBila shaka yoyote, siri ya utauwa ni kubwa: Alidhihirishwa katika mwili wa kibinadamu,
akathibitishwa kuwa na haki katika Roho,
akaonekana na malaika,
akahubiriwa miongoni mwa mataifa,
akaaminiwa ulimwenguni,
akachukuliwa juu katika utukufu.
Copyright information for SwhKC